FARID MUSSA ASEMA MBWANA SAMATTA AMEIBARIKI SAFARI YAKE YA KUCHEZA SOKA LA KULIPWA ULAYA

ALIYEKUWA winga wa timu ya Azam FC, Farid Mussa ambaye hivi sasa anaitumikia timu ya Tenerife inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Hispania, amefichua kwamba miongoni mwa watu wanaomtia moyo katika safari yake ya kucheza soka la kulipwa ni pamoja na nahodha wa timu ya Taifa Stars, Mbwana Samatta.

”Ninafanya mawasiliano ya mara kwa mara na Samatta ninapokuwa Ulaya, amekuwa msaada mkubwa kwangu kwa kunitia moyo wa uvumilivu ili niweze kustahimili mazingira magumu ya upweke barani Ulaya," alisema Farid.

“Samatta anayafahamu zaidi mazingira ya Ulaya kuliko mimi, hivyo nimekuwa nikitumia kama msaada kwangu katika mambo mbalimbali yanayozidi upeo wangu huko ughaibuni," aliongeza winga huyo.

Kulikuwa na hali ya sintofahamu kwa kipindi kirefu kabla ya winga huyo hajatimkia Ulaya ambapo ilionekana kama mpango usingefanikiwa na kuleta gumzo kwa taifa baada ya kimya kirefu kutanda.


Hata hivyo bado winga huyo hajafanikiwa kuanza kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo huku ikidaiwa kwamba ni kutokana na masuala ya utimamu wa mwili kuweza kukabiliana na mikikimikiki ya Ulaya.

No comments