FRANK LAMPARD ASEMA POGBA NI TATIZO MANCHESTER UNITED

 KIUNGO wa zamani mwenye heshima kubwa katika klabu ya Chelsea, Frank Lampard amesema kwamba usajili uliofanywa na Manchester United kwa Paul Pogba ni matatizo.

Amesema kwamba kama kuna matatizo yanayoisumbua Manchester United kwa sasa ni pamoja na usajili wa kiungo huyo akisema kwamba ulifanywa kwa sifa tu bila kuangalia uhalisia.

Nyota huyo amerejeshwa katika kikosi cha kocha Jose Mourinho kwa usajili wa kufuru wa euro mil 105 na hadi sasa hajafanya kile kinachoweza kuthibitisha thamani yake.

Mfaransa huyo hajaonyesha makali yake aliyokuwa nayo katika klabu ya Juventus alikotokea, kiasi cha kumfanya aseme kwamba Pogba ni tatizo katika kikosi cha Man United.

“Huzioni pauni mil 90 ambazo ni sawa na euro 105, huoni wapi zimepelekwa kila ukimtazama Pogba, naona kama fedha hizo zimetupwa ingawa najua Mourinho anaweza kurekebisha hali hiyo, lakini wakati haupo,” alisema Lampard akihojiwa na Sky Sports.

Amesema kwamba mchezaji mwenye thamani hiyo anatakiwa kuonyesha hali halisi ya fedha ambazo amelipwa tofauti na anachokiona kwa sasa kwenye miguu ya Mfaransa huyo.

Pogba amefunga mabao saba na kusaidia mengine matano katika mechi 38 ambazo amecheza msimu huu na Lampard amesema kwamba wastani huo ni mbaya na hauna uwiano na kiasi ambacho amenunuliwa kutoka Juventus.

No comments