HAMAD JUMA KUENDELEA KUILINDA NAFASI YA BUKUNGU SIMBA SC

BAADA ya beki wa pembeni, Janvier Bukungu kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Yanga, kocha wa Simba, Joseph Omog amesema ataendelea kumpa shavu Hamad Juma ili kucheza nafasi hiyo hadi hapo Bukungu atakaporejea dimbani.

Akiongea na Saluti5, Omog alisema kikosi chake kina wachezaji zaidi ya mmoja katika kila namba na anachokifanya ni kumweka tayari beki huyo kwa ajili ya mapambano.

Omog alisema mechi zote kwake ni muhimu, hivyo anawaandaa wachezaji wake kucheza kwa juhudi iliyokuwa katika mchezo uliopita.

“Nafikiri Hamad atacheza nafasi ya Bukungu, anaweza kucheza nafasi hiyo. Kikubwa ni kumsisitiza kuongeza umakini pale anapoona wapinzani wanakuja kushambulia,” alisema kocha huyo wa zamani wa Azam FC ya jijini Dar es Salaam.

Alimtaja mchezaji mwingine beki wa kati, Method Mwanjali kuwa bado hajaanza mazoezi wakati Mganda Juuko Murshid ameshaanza kujifua na wenzake.


Wekundu wa Msimbazi ndio vinara wa Ligi hiyo wakiwa na pointi 54, wakati mahasimu wao, Yanga wanakamata nafasi ya pili wakiwa na pointi 53.

No comments