HAZARD AZIONYA TIMU PINZANI KWA CHELSEA… asema kikosi chao kina uzoefu wa kutosha kung’ng’ania kileleni

STRAIKA Eden Hazard amezionya timu pinzani kwa Chelsea katika mbio za kuwania ubingwa akisema kuwa kikosi chao kina uzoefu wa kutosha kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi hadi mwishoni mwa msimu huu.

Kwa sasa vijana hao wa kocha Antonio Conte wapo kileleni mwa msimamo huo wa Ligi wakiwa mbele kwa pointi 10 dhidi ya Tottenham inayoshika nafasi ya pili, wakishukuru ushindi wa mabao 3-1 walioupata mwishoni mwa wiki dhidi ya Swansea City ikiwa ni wa 20 katika michezo 26 ya mechi za Ligi.

Manchester City wanaweza kupunguza pengo la pointi likabaki la point inane endapo watashinda kiporo chao na kocha Conte tayari ameshasema kuwa bado wanahitaji nyingine 29 ili kujihakikishia ubingwa ukiwa ni wa pili ndani ya misimu mitatu.

Hata hivyo, Hazard ambaye kiwango chake ndicho kilichosaidia timu hiyo kutwaa ubingwa msimu wa 2014/15, haamini kama kikosi chao kinaweza kuteteleka katika kipindi cha mwishoni mwa msimu huu.

“Sisi ni wataalam, tulitwaa ubingwa miaka miwili iliyopita kwa hiyo tunafahamu tunachokifanya,” alisema winga huyo.

“Tumekaa kileleni katika kipindi cha miezi ya kwanza msimu huu na hivyo tunahitaji kuendelea kukaa mahali hapo na tutafanya hivyo kwa kila mchezo,” aliongeza.

No comments