INIESTA ASEMA ANAFURAHISHWA NA NAMNA KOCHA LUIS ENRIQUE ANAVYOIONGOZA BARCELONA

STAA Andres Iniesta amesema kuwa anafurahishwa na jinsi kocha wao, Luis Enrique anavyokiongoza kikosi cha Barcelona na akasema kuwa ana matumaini ataendelea kuinoa klabu hiyo ya Camp Nou.

Luis Enrique anatakiwa kuinoa Barca hadi mwishoni mwa msimu huu lakini kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Paris Saint-Germain mapema mwezi uliopita katika michuano ya Ligi ya Mabingwa ndicho kinachotia shaka kama ataendelea kubaki kwenye nafasi yake.

Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Leganes ulionekana kidogo kupunguza wasiwasi huo na ule wa bao la dakika za mwisho Lililofungwa na Lionel Messi katika mchezo wao dhidi ya Atletico Madrid uliopigwa Jumapili, ndio uliowarejesha mabingwa hao watetezi katika mbio za kuwania ubingwa wa La Liga kabla ya Real Madrid kuzinduka na kupata mabao 3-2 dhidi ya Villareal.

Iniesta alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Barca kilichocheza mtanange huo uliopigwa kwenye uwanja wa Vecente Calderon, kilichotumia mfumo wa 3-4-3 anasema kuwa Luis Enrique bado anahitajika kwenye kikosi hicho.

“Kuna maelfu kwa maelfu wanaompenda kocha lakini hawafahamu kama ataendelea kufundisha. Kwangu mimi nina matumaini ataendelea ili aweze kutupa ubingwa kama alivyokwishafanya,” alisema Mhispania huyo mkongwe ambaye aliisaidia Barcelona kutwaa ubingwa mara nane ukiwemo msimu uliopita.

“Mechi dhidi ya Atletico ilikuwa ngumu mno. Atletico walikuwa wakitaka kushinda, lakini kwetu sisi ushindi ulikuwa muhimu sana,” aliongeza.


Kwa sasa Barca ipo nyuma kwa pointi moja dhidi ya Real Madrid lakini inacheza mechi moja zaidi dhidi ya mahasimu wao.

No comments