JAMIE VARDY: NIMEJIBU KWA VITENDO SHUTUMA ZA KUTIMULIWA KWA KOCHA RANIERI

STRAIKA Jamie Vardy amesema anavyodhani amejibu vyema shutuma zilizokuwa zikielekezwa kwake kuhusu aliyekuwa kocha wao, Claudio Ranieri, baada ya kuifungia timu yake ya Leicester City katika mchezo wao wa juzi wa Ligi Kuu England ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Liverpool.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa King Power, straika huyo wa timu ya taifa ya England, Vardy alifunga bao lake la kwanza tangu Desemba 10, mwaka jana akisaidiana na Danny Drinkwater na hivyo kuwafanya mabingwa hao watetezi kujikwamua katika ukanda wa kushuka daraja, zikiwa ni siku nne tangu alipofukuzwa Ranieri.

“Tulikuwa katika shutuma nzito kupitia vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii,” straika huyo aliiambia Sky Sports.

“Umeweza kuona vijana walivyokuwa wakitaka kujibu shutuma hizo na sasa imebaki kwetu. Ila siwezi kukumbuka ni kwanini Leicester City walikuwa wakicheza kwa kiwango kibaya na siwezi kumnyooshea kidole yeyote kwa hilo,” aliongeza nyota huyo.

Alisema kwamba kwa sasa anachotaka ni kujituma zaidi ili kuhakikisha anaibeba timu.

No comments