JERRY MURO ASIKITIKA YANGA KUMWACHIA KOCHA PLUIJM AENDE

KUONDOKA kwa aliyekuwa kocha na baadae mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, Hans Van Der Pluijm kumemfanya aliyekuwa msemaji wa klabu hiyo, Jerry Muro kushindwa kuvumilia na kutoa ya moyoni.

Jerry Muro alinukuliwa na kituo kimoja cha radio akielezea masikitiko yake kutokana na uongozi wa klabu hiyo kumwacha kocha huyo.

Muro alisema, kwa muda mchache aliokaa na Pluijm amebaini kuwa kocha huyo ni mmoja wa makocha bora zaidi kuwahi kuinoa Yanga, hivyo anasikitika kuona akiachwa.

“Kwa kweli mimi kama mwanachama wa yanga ninasikitika kuona uongozi umemwacha kocha Pluijm,” alisema.

Alisema, hakubaliani na sababu zilizotolewa na uongozi kuwa Pluijm ameachwa kutokana na klabu hiyo kuyumba kiuchumi.

Muro alisema, Pluijm aliyetua Singida United na kusaini mkataba wa kuinoa kwa miaka miwili timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu, ameacha pengo kubwa Yanga.

Alisema, kwa mtazamo wake kocha huyo alikuwa akihitajika zaidi kuendelea kuwepo Yanga kwani licha ya kuinoa lakini alikuwa mtetezi wa maslahi ya wachezaji, jambo lililofanya chini yake timu kufanya vyema kwani wachezaji walijituma uwanjani.

No comments