KAPOSHOO ‘NYOTA WA MCHEZO’ FM ACADEMIA MANGO GARDEN …atunzwa mshiko si wa kitoto

Licha ya mambo mengi mazuri yaliyopamba onyesho la FM Academia, ikiwemo utambulisho wa wanenguaji wapya, lakini ni tukio la mpiga tumba Kaposhoo ndiyo lililosisimua zaidi.

Katika onyesho hilo ndani ya Mango Garden, Kaposhoo akatambulishwa rasmi kama mpiga tumba mpya wa FM Academia na kuzua shangwe nyingi.

Kapashoo akazigonga tumba zake kwa ‘sifa’ na kuwafanya watu waamke kwenye viti vyao na kwenda kumtunza pesa kibao.

Ama kwa hakika Kaposhoo aliuthibitishia umma wa mashabiki wa muziki kuwa tumba zina ladha yake na zina wapigaji wake na wapigaji wenyewe ndio kama yeye.
Rais wa FM Academia Nyoshi el Saadat akamkaribisha rasmi kundini Kaposhoo na kumwambia atakula mbivu iwapo atatulia na kuwa mvumilivu.

“Tunajua watu kama nyie mna ukorofi wenu na hatujali kama huko ulifukuzwa au uliondoka mwenyewe, lakini sisi tunakupokea na ujisikie uko nyumbani. Umetuomba na sisi tumekupokea,” alisema Nyoshi.

Kaposhoo ambaye ana ulemavu wa ‘mwendo’ alikuwa akiitumikia Twanga Pepeta kabla hajasimamishwa na baadae kuondolewa kabisa kundini kwa kile kilichodaiwa kuwa bendi yake hiyo ya zamani haihitaji tena mpiga tumba kwa sasa.

Saluti5 tunasikitika kuwa kwa muda huu tumeshindwa kukuwekea picha za Kaposhoo jukwaani kutokana na hitilafu ya 'memory card' iliyotutokea baada ya kupiga picha nyingi za tukio hilo. Juhudi za kuokoa picha zinaendelea kufanyika.

No comments