KIKOSI CHA YANGA SC CHAKWEA PIPA KUIFUATA ZANACO ZAMBIA LEO

KIKOSI cha Yanga SC kinaondoka jijini Dar es Salaam leo Alhamisi kwa ndege ya Shirika la Kenya kwenda Lusaka, Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano hatua ya 32 bora Ligi ya mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Zanaco.

Katibu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa “Master” amesema katika mazungumzo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba msafara huo utakuwa na wachezaji 20 pamoja na viongozi kadhaa ambao watatajwa baadae.

Yanga ilianza mazoezi juzi asubuhi kujiandaa na mchezo huo wa marudiano baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na mabingwa hao wa Zambia katika mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa juzi uliochezeshwa na refarii kutoka Djibouti, Djamal Aden Abdi aliyesaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime, Yanga walitangulia kwa bao la winga wao machachari, Simon Happygod Msuva dakika ya 39, kabla ya Zanaco kusawazisha dakika ya 7 8 kupitia kwa mshambuliaji wao Mghana, Attram Kwame.


Yanga sasa watalazimika kwenda kushinda ugenini katika mchezo wa marudiano mwiashoni mwa wiki ili kusonga mbele hatua ya makundi.

No comments