KOCHA ARSENAL WENGER KUMRITHI ZINEDINE ZIDANE REAL MADRID

KWA lugha nyepesi unaweza kusema kuwa ni kama imefichuka baada ya kubainika kuwa kocha Arsene Wenger atakwenda kujiunga na timu ya Real Madrid endapo ataitema Arsenal wakati wa majira haya ya joto.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Telegraph, Mfaransa huyo kwa sasa anajiandaa kwenda kumrithi Zinedine Zidane katika vinara hao wa La Liga endapo Gunners wataamua kubadili kocha ifikapo mwishoni mwa msimu huu.

Mbali na hilo, taarifa za gazeti hilo zilieleza jana kwamba Wenger ana nyaraka za kuongezewa mkataba wa miaka miwili mezani na nyongeza ya mshahara ya pauni mil 10 kwa mwaka kutoka pauni mil 8 anazopata kwa sasa.

Taarifa zilikwenda mbali zaidi zikidai kwamba kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 vilevile amekataa ofa ya pauni mil 30 kwa mwaka kutoka moja ya klabu kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu ya China, Chinese Super League ili aweze kujiunga na vinara hao wa Hispania endapo hali hiyo itajitokeza.

Taarifa hizo zimekuja wakati Wenger akiwa bado hajaweka wazi hatima yake Arsenal licha ya kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Mapema mwezi uliopita Wenger alisema kuwa hatastaafu kufundisha soka mwishoni mwa msimu huu hata endapo kibarua chake cha kuinoa Arenal kitamalizika.


“Hakuna kitu kitakachojitokeza, msimu ujao nitaendelea kufundisha soka iwe hapa ama mahali pengine,” alikaririwa kocha huyo akisema katika vyombo vya habari.

No comments