KOCHA WA BARCELONA ASEMA HATMA YA INIESTA IKO MIKONONI MWA INIESTA MWENYEWE

KOCHA wa Barcelona, Luis Enrique amesema kwamba nyota wake Andres Iniesta ndio mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yake kwenye klabu hiyo ya Camp Nou.

Kauli ya kocha huyo imekuja baada ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 ambaye mkataba wake unamalizika mwakani, wiki iliyopita kusema kuwa atasaini mkataba mpya endapo atajisikia bado ni mchezaji muhimu kwa mabingwa hao wa La Liga.

Taarifa kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa Iniesta tayari ameshakataa ofa mbili kutoka kwenye klabu za nchini China “Chinese Super Legue” likiwemo dili ambalo ingeshuhudiwa akikinga kitita cha euro mil 35 baada ya kukatwa kodi.

Kutokana na hali hiyo, Luis Enrique anaamini mshindi huyo wa Kombe la Dunia na Mataifa ya Ulaya huenda akafikiria kutafuta changamoto mpya kama alivyofanya Xavi wakati mwaka 2015 alipoondoka na kwenda kujiunga na timu ya Al Sadd, lakini bosi huyo wa Barca anadhani hatma ya kiungo huyo ipo mikononi mwake mwenyewe.

“Nadhani mwanzoni mwa msimu tuliona mchango wa Iniesta, lakini baadae akakumbwa na majeraha makubwa mawili,” kocha huyo aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.


“Na sasa tunaangalia arejee tena katika ubora wake na anaelekea kutufanyia mengi,” aliongeza kocha huyo.

No comments