KUMBE BENNO VILLA ANTONY, TOTO TUNDU, SHAKASHIA WAKO TAYARI KUREJEA VIJANA JAZZ!

IMEFICHUKA kuwa wanamuziki Benno Villa Antony, Mhina Panduka “Toto Tundu”, Miraji Shakashia, na James Mawila, wangesharejea Vijana Jazz Band kama si viongozi wa juu kutotilia mkazo kuirudisha bendi hiyo kongwe kwenye ubora wake.

Kiongozi wa wakongwe hao, Sabuli Athuman amebainisha hayo alipohojiwa na Saluti5 iliyotaka kuthibitisha madai ya kuwa, baadhi ya wasanii wa Vijana Jazz hawako tayari kuruhusu wanamuziki wengine wenye uwezo kutua katika bendi hiyo kwa ajili ya kuiongezea makali.

“Tatizo haliko kwetu bali ni viongozi wa juu huko makao makuu (Umoja wa Vijana), ndio wanaoonekana kutupuuza na kutotupa uzito, lakini sisi kama wanamuziki tuna uchungu na bendi na tunafanya bidii ya kuongea na wanamuziki kila uchao ili kuona kama wanaweza kujiunga nasi ili kuongeza nguvu,” amesema Sabuli.

Hivi karibuni, kiongozi mstaafu wa Vijana Jazz, Rashid Pembe “Professor” alinukuliwa na mtangazaji wa kipindi cha Afro Tz cha radio One Stereo, Rajab Zomboko akisema kuwa inavyoonekana wanamuziki wa bendi yake hiyo ya zamani hawako tayari kuiruhusu wanamuziki wakali kujiunga nao ili kuleta mabadiliko.  

No comments