LIPULI FC YA IRINGA YATEMBEZA BAKULI KWA WANANCHI

UONGOZI wa timu ya Lipuli ya Iringa umewaomba wadau wa soka nchini kwa ujumla kujitolea chochote kwa ajili ya kuiwezesha timu hiyo kuanza maandalizi.

Akizungumza na Saluti5 kwa njia ya simu kutoka Iringa, Meneja wa timu hiyo, Mrisho Selemani alisema kutokana na timu hiyo kutokuwa na mfadhili wala wadhamini, wanaombwa wananchi wote wasaidie.

Alisema, kikosi chao ni kizuri lakini kinahitaji maboresho kidogo na maandalizi ya mapema ili waweze kuhimili ushindani katika Ligi Kuu.

“Tunawaomba wakazi wote na wenyeji wa Iringa walioko mikoa mingine tuungane kuisaidia timu yetu ianze maandalizi ya mapema,” alisema Selemani.

Alisema, mikakati yao ni kuhakikisha wanakiboresha kikosi lakini wakiendelea kuwakumbatia wachezaji walioipandisha daraja timu hiyo.


Lipuli imefanikiwa kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupita miaka 19 na Selemani anaamini kuwa sasa ni muda mwafaka kwa wana Iringa kujivunia vijana wao.

No comments