MAJERUHI YA PAUL POGBA YAMPA NAFASI NYOTA WA AC MONACO TIMU YA TAIFA UFARANSA

KOCHA wa timu ya taifa Ufaransa, Didier Deschamps amemuongeza katika kikosi chake nyota wa As Monaco, Tiemoue Bakayoko kwa ajili ya mechi ya kufuzu michuano ya fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Luxembourg na ya kirafiki dhidi ya Hispania, baada ya kiungo wake mshambuliaji, Paul Pogba  kulazimika kujitoa kutokana na majeraha ya misuli ya nyama za paja yanayomkabili.

Pogba alikumbwa na majeraha hayo wiki iliyopita wakati wa mechi ya Manchester United ya michuano ya Ligi ya Europa ambayo mashetani hao wekundu waliondoka na ushindi dhidi ya Rostov na atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili.

Kutokana na kukosekana kwa nyota huyo wa Man United, wamempa mwanya Deschamps kutafuta mbadala wake na sasa Bakayoko mwenye umri wa miaka 22 ameweza kupata fursa hiyo ya kucheza kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya wakubwa.

Jumatano wiki iliyopita Bakayoko alifunga bao tamu ambalo liliipa Monaco ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester City ambao uliifanya ishuhudiwe wakitinga hatua ya nane bora.

“Didier Deschamps amemuita nyota wa Monaco, Tiemoue Bakayoko kutokana na Paul Pogba kujiondoa baada ya vipimo vya madaktari kudhibitisha kuwa hataweza kucheza kwa muda wa siku 15,” ilisomeka taarifa fupi iliyotumwa kwenye tovuti ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo.


Kikosi cha timu ya Taifa ya Ufaransa, kitafunga safari Machi 25, mwaka huu kwenda nchini Luxembourg kabla ya kuivaa Hispania siku tatu baadae.

No comments