MANYIKA PETER ACHOSHWA NA BENCHI SIMBA SC… ajiandaa kusepa mwishoni mwa msimu

GOLIKIPA namba mbili wa Simba, Manyika Peter huenda akaachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya baba yake kumtaka kutafuta timu ambayo atapata nafasi ya kucheza.

Manyika amevumilia kwa muda mrefu lakini kwa sasa amepoteza matumaini kutokana na maisha yake yote kuishia benchi, jambo ambalo linamvunja moyo wa kuendelea kuichezea timu hiyo akihofia kupoteza kipaji chake.

“Baba amenishauri mwishoni nitafute timu nyingine ya kuchezea, kwasababu kuendelea kubaki Simba ni sawa na kuua kipaji changu, muda mwingi nakuwa benchi hata kwenye mechi za kirafiki, kipa anayepangwa ni Mghana Daniel Agyei,” amesema Manyika.

Kipa huyo amesema anafikiri kutekeleza ushauri wa mzazi wake kwa sababu ni kweli kiwango chake kimekuwa kikipungua siku hadi siku, jambo linalosababishwa na kutocheza mechi za ushindani ukiacha mazoezini.

Amesema kama mchezaji mdogo, ana ndoto za kufanya vizuri kwenye nafasi hiyo langoni lakini anashangazwa na mabosi zake, Joseph Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja kumfungia vioo huku wakimsotesha benchi.

“Inauma kuona msimu umebakiza mechi sita halafu sijacheza hata mechi moja, na mbaya zaidi wengine wanakuja na kupata nafasi huku mimi nikiendelea kuwa mchezaji wa mazoezini kwani hata mechi za Kombe la FA au zile za kirafiki sipangwi,” amesema Manyika.

Kipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika amesema atamuondoa mwanawe, Manyika Peter kudakia Simba kutokana na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Joseph Omog.


Manyika alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari baba yake mzazi, Peter Manyika ambaye amewahi kuichezea timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” na klabu ya Yanga, amemuhakikishia kumtafutia timu ya kucheza itakayompa nafasi katika kikosi cha kwanza.

No comments