MATOKEO YA SARE YA YANGA, ZANACO YAZUA JAZBA KWA MASHABIKI


MATOKEO ya sare ya kufungana bao 1-1 waliyoyapata Yanga juzi dhidi ya Zanaco FC ya Zambia katika mechi ya Ligi ya mabingwa Afrika “Total CAF Champions League”, yamewashitusha wengi.

Wakizungumza kwa hamaki baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam, baadhi ya mashabiki walisema hawana tena matumaini ya kuona timu hiyo ikitinga hatua ya makundi.

Walisema, wameshangazwa na mbinu zilizotumiwa na kocha George Lwandamila kuamua kucheza mchezo wa kujihami katika mchezo huo baada ya kushambulia.

“Kwa kweli, matokeo haya ya leo (juzi), yanatufanya tuishie hapa, sidhani tena kama tunaweza kushinda mchezo wa marudio na kufikia hatua ya makundi,” alisema Sallehe Mohammed wa tawi la Keko.

Akiungwa mkono na wenzake, Omary alisema hawajajua malengo ya kocha yalikuwa nini katika mchezo huo, lakini wanadhani sare inawaweka katika nafasi ngumu kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa ugenini Jumamosi hii.


Iwapo Yanga itashinda mechi ya marudiano itajikatia tiketi ya hatua ya makundi ambayo kwa mara ya kwanza itashirikisha timu 16 badala ya nane na ikishindwa itaangukia kwa mara nyingine katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

No comments