MBAO FC WAANZA TAMBO... wadai wako tayari kupambana na timu yoyote itakayokatiza mbele yao

UMEMSIKIA kocha wa timu ya Mbao FC ya jijini Mwanza, Etiene Ndaliyagije raia wa Burundi, jamaa anasema yuko tayari kupambana na timu yoyote itakayokatiza mbele yao.

Kocha huyo ameyasema hayo baada ya kufanikiwa kuing’oa Toto African na kutinga robo fainali ya Kombe la FA.

Timu hizo zilishuka dimbani Jumapili iliyopita na kutoka sare ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo, ndipo Mbao wakafanikiwa kusonga mbele kutokana na changamoto ya mikwaju ya penati wakiichapa Toto 4-2.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ikiwemo kukanusha kubebwa na waamuzi, alisema anashangazwa na malalamiko hayo ya Toto African kwani timu hiyo ingekuwa na uwezo ingeshinda ndani ya dakika 90.

“Kama Toto walikuwa na uwezo wa kushinda mbona hawakufanya hivyo, hawakufunga hata bao moja likakataliwa, kumbuka sisi kwenye Ligi tuliwafunga na tutakutana tena wiki ijayo (wiki hii), katika mechi ya Ligi Kuu na tutawafunga,” alitamba na kuongeza.

“Sasa hivi vijana wangu wanajiamini zaidi, wamebaini kuwa wakijitolea kwa pamoja tunaweza kufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu na hili ndio lengo letu,” alisema.


Alisema, kiu yake ni kuhakikisha timu hiyo ngeni inabaki Ligi Kuu ili apate muda wa kutosha wa kujipanga kwa ajili ya ushindani wa msimu ujao.

No comments