MICHAEL ESSIEN AANGUKIA LIGI KUU YA INDONESIA

KIUNGO wa zamani wa Chelsea na Real Madrid, Michael Essien ambaye amewahi kufananishwa na “greda” katika klabu hizo, amejiunga katika Ligi Kuu ya Indonesia.

Raia huyo wa Ghana amesaini mkataba wa miezi 12 na timu ya Persib Bandung ambayo inashiriki Ligi Kuu ya nchini humo.

Essien amesaini mkataba huo wa mwaka mmoja Jumatatu wiki hii wenye masharti ya kuongezwa akiwa katikati ya msimu kama atakuwa katika kiwango kikubwa.

Klabu hiyo ya Essien ndio ya mwisho kutwaa taji la ubingwa wa nchi hiyo mwaka 2014 na baadae Indonesia kukumbwa na adhabu ya FIFA ya kusimamisha shughuli za soka kwa miaka miwili.

Akiongea baada ya kusaini mkataba huo, Essien amesema kwamba anaamini wachezaji wengine wenye majina makubwa wataenda kuimarisha Ligi Kuu ya nchi hiyo.

“Naamini huu ni mwanzo mzuri kwa Ligi ya Indonesia na klabu ya Persib. Nawashukuru kwa kunileta hapa nami nawaahidi kwamba nitawaonyesha ubora wangu,” amesema.

Nyota huyo wa taifa wa Ghana, licha ya kung’ara kwa muda mrefu katika klabu ya Chelsea, pia amefanya vizuri kwenye klabu za Real Madrid, AC Milan na Panathinaikos.


Essien amecheza mara 256 katika Chelsea kwenye mashindano yote na baadae akatolewa kwa mkopo Real Madrid katika msimu wa 2012/13 na baadae akajiunga na AC kisha akatimkia Panathinaikos.

No comments