MTOTO WA STEVEN MAUFI WA SIKINDE AMLALAMIKIA BABA YAKE KUMBANIA KIMUZIKI KISA BONGO FLEVA

MTOTO wa mcharazaji gitaa la Solo wa Sikinde Ngoma ya Ukae, Steven Maufi, Jackson Steven Maufi amemchana baba yake kwamba amekuwa akimnyima ushirikiano kila pale anapomfuata na kumwomba ushauri wa kimuziki.

Akiongea nyumbani kwake, Tabata Makuburi, jijini Dar es Salaam, Jackson ambaye ni msanii chipukizi wa bongo fleva amesema kuwa baba yake huyo amekuwa akimdhihaki na kuwambia hawezi kumsaidia kwavile muziki anaoufanya (bongofleva), ni wa uongo.

“Mama ndio amekuwa akinisaidia na kunipa moyo unaonifanya nizidishe kasi katika muziki, lakini baba huwa ananambia kuwa hawezi kujishughulisha na muziki wangu wa uongo, labda hadi hapo nitakapoamua kujitupa kwenye dansi,” amesema.


Saluti5 ilipomtafuta Steven Maufi mwenyewe na kumuuliza juu ya madai ya mwanae, amesema kuwa hajawahi kumfuata kwa nia ya kumtaka amsaidie kimuziki na kwamba wala hajui kuwa mwanae huyo ni msanii.

"Mwanangu anaishi na mama yake, sijui kabisa kama ni msanii," alisema Maufi.

No comments