MWIGIZAJI LINDSAY LOHAN WA MAREKANI AWATEMBELEA NA KUWAFARIJI WAKIMBIZI WA SYRIA

MWIGIZAJI mahiri wa kike kutoka Los Angeles, Marekani, Lindsay Lohan amewatembelea, kuwapa misaada na kuwafariji wakimbizi wa Syria walioko nchini Uturuki.

Lohan mwenye miaka 30, alitumia muda mwingi kuzungumza na wanawake na kuwafariji watoto walioko kwenye kambi za wakimbizi, huku akitoa wito wa dunia kuona umuhimu wa kukomesha vita Syria.

Aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa hali aliyowakuta nayo wakimbizi hao ni ya kuhuzunisha, achiliambali namna watoto wengi wanavyokumbwa na kiwewe kutokana na kukumbuka jinsi wazazi na jamaa zao walivyouawa kikatili.

Alisema, alilizwa na mtoto Hussein ambaye alimweleza kuwa alimshuhudia baba yake, Mohammad akipigwa risasi kadhaa na kufariki dunia walipokuwa nyumbani kwao mjini Aleppo.

Pia kisa cha binti aitwaye Heya mwenye miaka tisa, ambaye ni pacha na mwenzake wa kiume aitwaye Leys, aliyesema wamepoteza wazazi wote na kwa sasa wapo katika uangalizi wa kaka yao mwenye miaka 17, ambaye analazimika kufanya vibarua ili kuwatafutia chakula na mahitaji mengine.


No comments