RIHANNA AMPIKU MICHAEL JACKSON TOP TEN YA MAREKANI

HATIMAYE mwanamuziki maarufu duniani, mrembo aliyejitosa kwenye mitindo na ubunifu wa mavazi, Rihanna amempiku Michael Jackson katika kuwa na nyimbo nyingi katika chati ya nyimbo 10 bora nchini Marekani.

Hii ni baada ya wimbo wake mpya wa “Love On The Brain” kuingia kwenye orodha hiyo.

Huo umekuwa wimbo wa 30 kwa Rihanna kuwa kwenye chati hiyo ya juu na sasa ameachwa nyuma na kundi la The Beatles pamoja na Lady Madonna.

Madonna ndie anayeongoza katika chati hiyo akiwa ameingiza jumla ya nyimbo 38 zilizopata kutamba kwa nyakati tofauti kwenye chati hiyo, wakati The Beatles wana nyimbo 34.

Michael Jackson aliyefariki dunia Juni, 2009 alikuwa na nyimbo 29 katika chati hiyo ya nyimbo 10 bora.

Mwaka 2005, wimbo wa Rihanna wa “Pon de Replay” ulikuwa namba mbili katika chati za muziki Marekani na Uingereza kwa mpigo.

Imechukua mwanamama huyo miaka 10, miezi saba na wiki mbili kuwa na nyimbo 30 kwenye chati ya nyimbo bora Marekani.

Nyimbo zilizovuma za Madonna alizichomoa katika kipindi cha miaka 13.

Mafanikio hayo yanakuja ikiwa ni karibu mwaka mmoja tangu Rihanna alipoweza kumfikia Madonna katika oroidha ya waimbaji wa kike wenye nyimbo nyingi zaidi katika chati ya 100 bora Marekani Julai, 2016.


Wakati Rihanna akisota kwa miaka 10 kuweza kuchomoka kwa upande wa kundi la The Beatles wao walifika hapo kwa kutumia miaka mitano, miezi tisa na wiki mbili pekee.

No comments