SUAREZ ASEMA HAKUTEGEMEA KAMA IKO SIKU ANGEPANGWA NAMBA YA LIONEL MESSI

STRAIKA wa Barcelona, Luis Suarez amefichua siri ya kwamba katika maisha yake hakuwa na ndoto ya kucheza katika timu moja na nyota wa dunia, Lionel Messi.

Lakini sasa anakiri kuwa ndoto ilipotimia aliinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa kutimia kwa hatua ya kusakata soka katika kikosi kimoja na supastaa huyo raia wa Argentina.

Kauli ya Suarez inakuja katika kipindi ambacho wakati mwingi kocha amekuwa akimpanga kucheza namba tisa ambayo ndiyo anayoitumia Messi, hatua ambayo amekiri kuimudu.

Alisema, kabla ya kujiunga na Barca akitokea Liverpool mwaka 2014, hakutarajia kucheza katika jukumu alilonalo Messi ingawa kwa sasa amekiri kufanikiwa.

Kwa nyakati kadhaa tofauti, Messi amekuwa nje ya kikosi cha Barca kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa majeruhi, lakini Suarez amekuwa akichukua nafasi yake na kucheza kama mshambuliaji wa kati.

“Sikuwahi kudhani hata kidogo kama nitacheza namba ambayo Messi hupangwa kutokana na uzoefu wake, yaani namba tisa. Lakini nimepangwa na nimemudu.”

“Nimekuwa nikipangwa namba tisa wakati Messi hayupo ama hata akiwepo tumekuwa tukicheza kwa kubadilishana wakati mchezo ukiendelea, hii ni hatua ya kujivunia.”

“Kucheza katika mfumo wa kujiamini na kupokezana kumesaidia timu kutomtegemea mchezaji mmoja katika idara ya ushambuliaji, ndio maana utakuta tunacheza kwa kupishana.”


“Ninaweza nikawa mimi baadae Messi na kisha Neymar, wote tumekuwa tukipangwa kulingana na aina ya mchezo na tumekuwa katika mfumo mzuri siku zote,” alisisitiza Suarez.

No comments