WANA BUKOBA WAMPIGIA DEBE MECK MEXIME ABAKI KAGERA SUGAR MUDA MREFU ZAIDI BAADA ya timu yao kuponea chupuchupu kwa misimu miwili mfululizo kushuka daraja, mashabiki wa Kagera Sugar wamempa tano kocha wao, Mecky Mexime na kutaka uongozi kumuongezea mkataba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya mashabiki hao walisema kuwa kocha huyo ameiwezesha timu hiyo kurejesha makali yake na wanaamini akipewa muda wa kutosha kuitengeneza, upo uwezekano wa kuandika historia ya kutwaa ubingwa.

Walisema, nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars ameifanya timu kuwa tishio licha ya kwamba iliuanza msimu kwa kusuasua lakini sasa wamekuwa na shauku ya kwenda uwanjani kila inapocheza.

“Kwa kweli Mexime ametupa raha sana wana Bukoba, hivi sasa timu ya Kagera Sugar ikicheza tunakwenda uwanjani kifua mbele kwani tunakuwa tuna uhakika wa ushindi, tunaomba aongezewe muda,” alisema Bakari Kamazima mbele ya wenzake.

Akiungwa mkono, wenzake walisema kuwa kutokana na umri wake, ni vyema uongozi ukafikiria kumpa mkataba walau wa miaka mitano ili nae aweze kuelekeza akili zake zote kuisuka timu hiyo kwa kutarajia mafanikio.

Alisema, kadri kocha anavyopewa muda mfupi ndivyo anavyoshindwa kutumia muda wake kupigania maslahi ya klabu, jambo ambalo limeonekana katika klabu nyingi hapa nchini.
 
Kagera Sugar kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu licha ya kwamba haina nafasi ya ubingwa wala nafasi ya pili, lakini ina uwezo wa kumaliza katika nafasi tano za juu ikiendeleza wimbi la ushindi katika mechi sita zilizobaki.

No comments