WENGER AFANANISHA UVUMI WA KWENDA FC BARCELONA NA UTANI UNAOPASWA KUPUUZWA

KAMA ukiamua kufanya mashindano ya mtu mbishi kuliko wote duniani, basi katika orodha yako usiache kumtaja kocha wa sasa anayetakiwa kuondoka ndani ya klabu ya Arsenal, mzee Arsene Wenger.

Kocha huyo amesema kuwa anasikia kuna ofa inamtaka kuondoka katika klabu yake ya sasa na kwenda kuwanoa FC Barcelona ya Hispania, lakini akasema kuwa kama kuna utani unaopaswa kupuuzwa basi ni pamoja na ofa hiyo.

Kwake yeye Wenger amesema kwamba anadhani hana muda wa kuzungumzia hatma yake kwa sasa wakati bado mkataba wake haujamalizika, lakini pia amepuuza madai kwamba ni lazima aondoke klabuni hapo.

Kocha huyo anatajwa kwamba anaweza kuhamia Barcelona kutokana na madai kwamba klabu hiyo inakaribia kuachana na kocha wake wa sasa, Luis Enrique.

“Sidhani kwamba barca ni mahali sahihi kwangu. Hata kama kweli nataka kuondoka Arsenal kama akili ikiniambia hivyo, lakini mahali pa kwenda sio Barcelona,” alisema Wenger.

Kocha huyo amesema kwamba anataka kuendelea kuipigania klabu yake ya sasa na kwamba wazo la kwenda kokote lingefutwa kwanza.

“Kama ukiniambia kwamba ninatakiwa kwenda Barcelona nitakujibu tu kuwa bora nifie hapa Arsenal, hata kama sio lazima kuwa kocha,” amesema.


Kauli hiyo ya Wenger inaondoa kabisa matumaini kwa Barcelona kwamba inaweza kumpata mzee huyo na sasa iangalie mahali kwingine.

No comments