WIMBO “HESHIMA IKO WAPI” WAMNG’ARISHA ZAIDI MWIMBAJI ATHUMANI KAMBI MSONDO NGOMA


MWIMBAJI Athuman Kambi ameonekana kung’ara zaidi ndani ya Msondo Ngoma Music Band baada ya kuachia kibao ‘Heshima Iko Wapi’ kinachovuta hisia za mashabiki wengi kila kinaporindimiashwa kwenye kumbi wanazopiga.

Ndani ya kibao hicho kilichobeba meseji kali kwa jamii, mwimbaji huyo wa sauti ya kwanza akishirikiana na wenzie, anaonekana kunogesha kwa mashairi mazito kiasi cha kuwapagawisha wapenzi wao wengi wanapokisikia.

Saluti5 iliyotembelea shoo za Msondo Ngoma kwa wiki kadhaa sasa, imeshuhudia namna mashabiki wanavyoshindwa kubaki vitini wakati kibao hicho kikipigwa na kujikuta wakijimwaga katikati kucheza na wengine kutuza.

Alipoulizwa, Kambi amesema kwamba wimbo huo ni tukio la kubuni na wala halihusiani na tukio lolote lililowahi kutokea, ingawaje kuna baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha na mikasa mbalimbali ya kweli ya kimaisha.


“Nashukuru kuona baadhi ya mashabiki na wadau wa muziki wameupokea wimbo huo vizuri, huku wengine wakiuhusisha na matukio ya kweli, najua huko ndiko kufanikiwa kwangu kama msanii wa kweli,” amesema Kambi.

No comments