YANGA WALIA NA RATIBA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema kuwa ratiba imekuwa ngumu kwao kutokana na aina ya michuano inayowakabili, lakini watajitahidi kupambana kuendelea nayo.

Mwambusi amesema hali ya majeruhi nayo imezidi kupoteza ubora wao, jambo ambalo nalo linaleta hofu ya kuweza kupoteza mechi muhimu.

“Ukweli tupo katika wakati mgumu sana, kwanza ratiba sio rafiki kwetu lakini hatuna namna na kingine tumekuwa na majeruhi wengi na tunawakosa wachezaji wengi kutokana na majeruhi,” amesema Mwambusi.

Kocha huyo amesema akili na fikra zao kwa sasa wanazielekeza kwenye michuano hiyo kwasababu wamepania kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ili kuweza kutinga hatua ya makundi kama walivyofanya msimu uliopita.

Amesema, pamoja na kuwa na kikosi kipana, lakini nyota ambao wanakosekana kuelekea mchezo huo ni muhimu sana kutokana na uzoefu walionao.


“Ni kweli Yanga tuna kikosi kipana lakini ubaya wake ni kwamba wachezaji waliopo licha ya kuwa na kipaji cha kucheza mpira, wanakosa uzoefu na hii ni michuano mikubwa inayohitaji uzoefu, lakini hadi kufikia sasa hakuna namna inatubidi twende kucheza,” amesema Mwambusi.

No comments