YANGA YAICHIMBA MKWARA AZAM FC... yaiambia isitarajie mchekea kama wa Zanzibar

APRILI Mosi mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameapa kuutumia mchezo wa marudiano dhidi ya Azam kama sehemu ya kulipa kisasi kufuatia kipigo ambacho Yanga walikipata kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kisiwani Zanzibar.

Yanga inashuka dimbani ikiwa pungufu kwa pointi mbili toka kwa vinara wa Ligi kuu Tanzania Bara, Simba ambao nao watakuwa na ziara kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuzidi kujikita kileleni.

Katika mchezo wa awali ambao ulitawaliwa na rafu uwanjani timu hizo zilitoka sare ya mabao 0-0 katika dimba la uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mkongwe wa timu hiyo, Nadr Haroub "Cannavaro" alisema kuwa Azam isitarajie kukutana na wepesi kama ambavyo walipata ushindi kwenye mchezo wao wa mwisho kule visiwani Zanzibar.

“Tunafahamu umuhimu wa mechi dhidi ya Azam ili tujiweke kwenye mazingira mazuri ya kutwaa  ubingwa hivyo tunalazimika kushinda kwa kila hali,” alisema beki huyo kutoka Zanzibar.

“Azam wana kikosi kipana na hawana tofauti kubwa kiuchezaji na sisi lakini kutokana na umuhimu wa mechi inatulazimu kushinda ili kuzidi kuitia presha Simba,” aliongeza beki huyo.

Naye kocha wa Yanga, George Lwandamina aliongeza kuwa kikosi chake kipo kwenye hali nzuri baada ya nyota wake kurejea toka kwenye majukumu ya kuzitumikia timu za taifa na majeruhi aliokuwa nao akiwemo Donald Ngoma na Amissi Tambwe raia wa Burundi kurejea dimbani.

“Tunafahamu ugumu wa mechi hii ambayo pia Simba wanaifatilia kwa ukaribu, lakini tunawaahidi wanachama wetu kwamba tutapambana mpaka mwisho ili kuibuka na ushindi,” alisema kocha huyo.


“Kikosi kipo katika hali nzuri kwa pambano letu la Jumamosi ya wiki hii hivyo tunaomba sapoti ya mashabiki uwanjani ili kuleta hamasa ya ushindi kwa wachezaji," aliongeza.

No comments