ABDI BANDA AIPA MATUMAINI SIMBA DHIDI YA AZAM FC JUMAMOSI

KUREJEA kikosini kwa beki wa kati wa Simba, Abdi Hassan Banda kumeongeza jeuri ya kujiamini kwa benchi zima la ufundi la wekundu hao na uhakika wa kuwaondoa wapinzani wao Azam FC watakapovaana Jumamosi hii kwenye mechi ya nusu fainali.

Kocha wa Simba, Joseph Omog amesema kwamba kurejea kwa Banda kunaongeza makali kwenye kikosi chake na sasa ni kama safu yake imekamilika na wako katika morari ya juu kupambana na Azam katika mechi hiyo ya keshokutwa.

Banda amerejea kikosini hivi karibuni akitoka kifungoni baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumfutia adhabu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavila.

Awali, Banda alisimamishwa na kamati ya saa 72 ya Shirikisho, ambapo aliikosa michezo miwili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC na Toto Africans kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Omog alisema kuwa amefurahi kuona beki wake ambaye ni tegemeo akirejea uwanjani kwenye mechi dhidi Azam baada ya adhabu yake kufutwa na kwamba sasa ukuta wake umekamilika, kwasababu pamoja na Banda, beki mwingine wa kati, Juuko Murshid yuko vizuri zaidi.

Omog alisema, kwenye mechi mbili ambazo beki huyo hakuwepo pengo lake lilionekana kutokana na umuhimu wake mkubwa kwenye kikosi chake kilichopanga kuchukua mataji mawili; Ligi Kuu na Kombe la FA.

“Sina hofu na kikosi changu kuelekea mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA tutakapokutana na Azam Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa, kwani nina furaha ya kurejea kwa Banda.”

“Kama unavyojua, Banda alikosa michezo miwili ya Ligi Kuu dhidi ya Mbao tuliowafunga mabao 3-2 na Toto African ambayo tulitoka suluhu, hivyo nina imani kubwa ya kupata ushindi kwenye mchezo huo.”


“Ninafahamu mechi itakuwa ngumu sana lakini kwa upande wetu Simba tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na tayari tumeziboresha baadhi ya nafasi zenye upungufu kuhakikisha tunavuka kisiki hiki cha kwanza tukisubiria Ligi Kuu,” alisema Omog.

No comments