AFANDE SELE ATOA SALAMU ZA POLE KWA BELLE 9

MKONGWE wa bongofleva, Selemani Msindi “Afande Sele” amempa pole msanii mwenzie wa miondoko hiyo, Belle 9, kufuatia kifo cha baba yake mzazi, Damian Nyamoga kilichotokea usiku wa kuamkia jana kwa kugongwa na pikipiki iliyokuwa kwenye mwendokasi.

Katika salamu hizo, Afande amemuomba Belle 9 kuwa mvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mpito, ingawaje anafahamu kwamba kufiwa na baba mzazi ni kati ya misiba mitatu mizito zaidi hapa duniani.

“Mdogo wangu Belle 9 nakupenda sana ndio maana nilipopata taarifa za msiba wa baba yetu kipenzi nilivunja shughuli zangu zote na kujumuika, ila tafadhali naomba punguza mawazo kwani hii ni njia yetu sote,” amesema Afande.

Mwili wa marehemu mzee Nyamoga umezikwa leo mchana hukohuko Morogoro Mjini alikokuwa akiishi na familia yake.

No comments