ALHAJI RAGE KUIONGOZA SIMBA SC FIFA KUDAI "HAKI" YA POINTI TATU

MWENYEKITI wa zamani wa Simba SC, Alhaji Ismail Aden Rage ni kama ameshatangulia kwenye Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kuipigania klabu yake hiyo ya zamani kwani inavyosemekana sasa huenda sakata la Simba kupokonywa pointi tatu likawakimbiza wekundu hao wa Msimbazi hadi Uswizi yalipo makao makuu ya FIFA kudai haki yao.

Rage ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa TFF wakati huo ikijulikana kama FAT, amesema maamuzi yaliyofanywa dhidi ya Simba yanaonyesha dhahiri uonevu na kwamba wakienda FIFA na Shirikisho la Afrika (CAF), watapata msaada.

“TFF wamekubali kama Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano na atakosa mchezo unaofuata, hii sheria ni mpya maana tunazozijua sisi, hasa ile ya kanuni namba 42 (11), inasema mchezaji mwenye kadi tatu za njano haruhusiwi kucheza mchezo unaofuata, lakini kama Simba walikuwa hawajalipa ada au rufaa yao imechelewa, kwanini wasingelitupiliambali kama kanuni zinavyoeleza?”

“Hii kanuni ya kusema Fakhi atakosa mchezo unaofuata ni mpya na haipo kokote kule, tunajua TFF ina uwezo wa kufanya marekebisho kwenye vifungu vyake vya katiba, ila si mwishoni mwa Ligi. Mimi nawashauri waende FIFA kutafuta haki yao,” alisema Rage.

Amesema, kwa jinsi jambo hilo lilivyokaa, yeye mwenyewe yuko tayari kupeleka malalamiko yanayohusu Simba katika vyombo hivyo vya juu.


Barua ambayo bodi ya Ligi wameiandikia Simba, inaonyesha kwamba beki huyo alikuwa na kadi tatu za njano na TFF pia imekiri hivyo katika hukumu yake ya wiki iliyopita.

No comments