ALLY CHOCKY: NIMESIMAMISHWA MIEZI MIWILI TWANGA KWA NJIA YA ‘MESEJI’ …BARUA ITAFUATA


Mwimbaji tegemeo wa Twanga Pepeta, Ally Chocky ameiambia Saluti5 kuwa amesimamishwa kazi Twanga Pepeta kwa miezi miwili.

Chocky amefichua kuwa adhabu yake itaisha tarehe 1 Julai, hii ikimanisha kuwa hatonekana kwenye jukwaa la bendi hiyo hata kwenye onyesho la Eid el Fitr.

Mwimbaji huyo anasema amesimamishwa kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi (SMS) iliyotumwa kwake na meneja Hassan Rehani.

Ingawa Chocky hakuweka wazi sababu za kusimamishwa kwake, lakini Saluti5 inafahamu kuwa maonyesho yake binafsi nje ya bendi, ndiyo sababu kuu ya adhabu hiyo.

Katika mkataba wake wa miaka mitatu ndani ya Twanga, Chocky alitakiwa kuomba ruhusa kwa njia ya barua pale anapotaka kufanya maonyesho yasihohusiana na na bendi yake.

Saluti5 imeelezwa kuwa ni maonyesho machache ambayo Chocky aliyaomba kwa barua, lakini mengine amekuwa akiaga kwa njia tofauti ambazo hazikidhi masharti ya mkataba.

“Nimeambiwa barua ya kusimamishwa imeshaandikwa, ikinifikia mkononi nitajua sababu kuu ya kusimamishwa kwangu,” alisema Chocky kwa njia ya simu jana mchana.

Meneja wa Twanga Pepeta, Hassan Rehani alipopigiwa simu na Saluti5 jana mchana, alikiri kuwa Chocky amesimamishwa lakini hawezi kuongea kwa undani kwa kuwa yeye si msemaji wa jambo hilo.

Chocky ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, hakushiri maonyesho ya Twanga Pepeta katika msimu wa sikukuu ya Pasaka na badala yake alikuwa na maonyesho yake binafsi Tanga mjini na Handeni.

Uchunguzi wa Saluti5 umebaini kuwa adhabu hiyo ya Chocky itakuwa ni ya bila malipo.

No comments