BARCELONA YAONGOZA LIGI BAADA YA KUICHAPA REAL MADRID … Sergio Ramos alambwa red card, Messi usipime


Barcelona inaongoza La Liga kwa tofauti ya magoli baada ya kuinyuka Real Madrid 3-2 katika ‘El Clasico’ iliyopigwa Santiago Bernabeu.

Nahodha wa Barcelona, Lionel Messi aliyekuwa akichezewa rafu za mara mara, ndiye aliyeibuka kuwa nyota wa mchezo kwa kudumbukiza wavuni mabao mawili.

Real Madrid walikuwa wa kwanza kufunga dakika ya 28 mfungaji akiwa Casemiro lakini Messi akachomoa dakika 33 na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa 1-1.

Pengine hadithi ingekuwa nyingine kama Cristiano Ronaldo asingepoteza nafasi ya dhahabu aliyoipata dakika 68 baada ya Asensio kumpenyezea mpira Benzema aliyetoa krosi kwa Ronaldo lakini kwa mshangao wengi akapaiza mpira ndani ya kisanduku cha sita huku kipa Stegen akiwa kishapotea njia.

Barcelona wakapata bao la pili kwa  mkwaju mkali wa kiungo Ivan Rakitic kunako dakika ya 73 huku dakika mbili baadae Real Madrid wakifanya jaribio la kusawazisha kwa shambulizi lililioshia kwa Ronaldo kupiga shuti la umbali wa mita 20 lakini kipa Stegen alisimama imara na kuokoa.

Real Madrid wakapata pigo dakika ya 77 baada ya sentahafu wake Sergio Ramos kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya Messi.

Licha ya kucheza pungufu, Real Madrid walimimina mshambulizi ya mfululizo yaliyozaa bao la kusawazisha dakika ya 86 mfungaji akiwa James Rodriguez.


Wakati ikionekana kama vile mpira utamalizika kwa sare ya 2-2, Messi akaifungia Barcelona goli la tatu dakika ya mwisho ya mchezo.

No comments