BEKI WA TOTO AFRICAN ADAI AMECHOMOA KUJIUNGA SIMBA SC... asema tayari "ameshafunga maneno" na Singida United

BEKI kisiki wa Toto African, Yusuph Mlipili ambaye alikuwa tatizo kubwa kwa washambuliaji wa Simba wakati timu hizo zilipokumbana kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Bara katika uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, anaonekana kuanza kuiweka Simba njia panda.

Mlipili amesema kwamba Simba walimfuata baada ya mechi kumalizika ili kumshawishi ajiunge nayo lakini aliweka wazi kuwa tayari timu ya Singida United alifanya nayo mazungumzo.

“Ni kweli kuna kiongozi wa Simba alinifuata baada ya mechi kuisha akajaribu kunishawishi nijiunge nao lakini nilimuweka wazi kuwa Singida United walitangulia kunifuata kabla yao,” alisema beki huyo.

“Sijui uelekeo ukoje mkataba wangu hapa uko mwishoni, naheshimu makubaliano niliyofanya na timu yangu hivyo ni mapema sana kuihakikishia Simba kuwa nitajiunga nayo ama la,” aliongeza beki huyo.


Mlipili alifanikiwa kuiongoza vyema safu ya ulinzi ya Toto African ambapo alidhibiti mashambulizi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa CCM Kirumba kwa kuisha kwa sare ya bila kufungana.

No comments