EMMANUEL OKWI AMMIMINIA SIFA LAUDIT MAVUGO... "abipu" kurejea Simba SC

MGANDA Emmanuel Okwi huyo ambaye kwa sasa anafanya vyema na kikosi cha SC Villa, amesema kwamba amekuwa akifuatilia mwenendo wa Simba lakini ameguswa sana na uwezo wa Laudit Mavugo.

Katika mahojiano na saluti5 kwa njia ya mtandao, Okwi amesema kwamba Mavugo ni mchezaji mzuri na kama atabaki Simba ni hadhina ya baadaye.

Okwi amesema kwamba amemfatilia mchezaji huyo raia wa Burundi na kugundua kwamba amekuwa msaada mkubwa kwa Simba.

“Nimemfuatilia sana yule jamaa hana papara uwanjani lakini ana uwezo mkubwa sana kama atabaki katika kikosi hicho itasaidia sana Simba katika michezo ijayo,” amesema.

Mganda huyo amesema kwamba kurejea kwake Simba siyo jambo la kushangaza na hasa ikizingatiwa kwamba ni katika klabu hiyo ambapo amepata mafanikio makubwa.

“Unashangaa kwamba mimi nataka kurejea Simba, hilo sio jambo la ajabu kwangu kwani Simba ni kama nyumbani kwangu katika maisha yangu ya soka, Simba ndiko nilikopata mafanikio makubwa,” amesema Okwi na kuongeza:

“Nimecheza Yanga, nimecheza Etoile du Sahel na nimekwenda Denmark lakini ukichunguza utaona kwamba Simba ndiko ambako nimecheza mpira kwa uhakika zaidi.”

Okwi amesema pia amefanya vizuri katika klabu ya Villa kwa sababu maishsa hapo hayana tofauti na yale aliyoishi Simba.


“Villa ndiyo wamenilea, Simba wakanikuza maisha ya Villa na Simba yanafanana sana ingawa kuna mambo madogo yametofautiana,”amesema.

No comments