GOTI LAMFANYIA KITU MBAYA THOMAS ULIMWENGU


IMEKUWA ni mkosi kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu ambaye aliamua kuachana na TP Mazembe na kutimkia Ulaya kukipiga na AFC Eskilstuna ya nchini Sweden,  lakini mambo yamekuwa magumu kwake kwasababu ya jeraha la goti ambalo bado linamweka nje ya kikosi.

"Bado sijaweza kuonyesha kiwango changu halisi, inaniumiza sana kuona nakaa nje ya kikosi kutokana na maumivu ya goti langu la mguu wa kushoto,” alisema Ulimwengu.

“Nina wakati mgumu kidogo, nilifanyiwa vipimo nikaambiwa natakiwa kukaa nje ya kikosi kwa miezi mitatu baada ya kuonekana kuna tatizo kwenye goti langu la kushoto,” aliongeza mshambuliaji huyo mwenye mwili mkubwa.

 Thomas Ulimwengu anabainisha wazi kuwa alihisi maumivu baada ya kuumizwa kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Malmo FF katika mchezo uliofanyika machi 23, mwaka huu.

“Nilihisi maumivu makali sehemu ya goti siku tulipokuwa kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Malmo, bado najiuguza mpaka hii leo sijaweza kucheza,” aliongeza.

Mshambuliaji huyo baada ya kupata mafanikio kwenye klabu ya TP Mazembe nchini Kongo akibeba ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika, aliamua kuachana na timu hiyo na kufuata hatua za Mbwana Samatta anayecheza timu ya Genk ya Ubelgiji.

No comments