HIMID MAO AITAHADHARISHA SIMBA MCHEZO WAO WA NUSU FAINALI YA FA JUMAMOSI

KIUNGO mkabaji wa Azam FC, Himid Mao Mkami “Ninja” ambaye aliifunga Simba bao muhimu kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar, ameibuka na kuitahadharisha timu hiyo kabla ya mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la FA keshokutwa Jumamosi.

Mao amesema kuwa dhamira yao ya kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ipo mikononi mwa Simba, hivyo watahakikisha wanafanya kila namna kuiondosha kwenye hatua hiyo.

“Kila mtu anajua kwamba tumewafunga mara mbili mfululizo, lakini hiyo haitufanyi tuiddharau Simba, kama wachezaji tutafanya sehemu yetu kuhakikisha tunaibuka na ushindi.”

“Tunajua wamepania lakini bado hilo haliwezi kukatisha mpango wetu wa kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema kiungo huyo aliyetoka kwenye familia ya soka.


Timu ya Azam inakumbana na Simba ikiwa ndio tumaini pekee la kushiriki michuano ya kimataifa, baada ya kuondoka rasmi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao upo mikononi mwa watani wao wa jadi Yanga.     

No comments