KAMBI YA SERENGETI BOYS YAPAMBA MOTO MOROCCO

TIMU ya taifa ya vijana “Serengeti Boys” bado inaendelea na kambi yake katika kituo cha soka cha Maamoura jijini Rabat, Morocco, ikiwa kama sehemu ya maandalizi kabla ya kuanza kivumbi cha AFCON huko nchini Ghana.

Serengeti Boys ambayo ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu nyumbani dhidi ya Burundi mara mbili wakishinda mabao 3-0 na 2-0 na dhidi ya Ghana wakitoka sare ya 2-2, baada ya kambi ya Morocco, kikosi hicho kitatimkia Yaunde, Cameroon kwa maandalizi ya mwisho ikiwemo michezo miwili ya kirafiki dhidi ya wenyeji, Mei 3 na 6, mwaka huu.       
“Kama unavyojua tuko hapa kwa muda mfupi kabla ya kutimkia Yaunde, lakini hali ya kikosi changu kwa kiasi kikubwa kimeimarika, tunashukuru juhudi zinazofanywa na shirikisho pamoja na michango mbalimbali toka kwa Watanzania,” alisema kocha Bakari Shime.

“Tunafahamu wazi jicho la Tanzania lipo kwetu hivi sasa, niwatoe hofu kuwa hatutakwenda kuwaangusha,” alimaliza kocha huyo.


Timu ya Serengeti Boys imepangwa kwenye Kundi moja na timu za Mali, Nigeria na Angola.

No comments