KIMENUKA KAGERA SUGAR... viongozi washikana uchawi kwa kadi tatu za Fakhi

KUMEZUKA sintomfahamu kubwa katika timu ya Kagera Sugar baada ya baadhi ya viongozi kulaumiana katika suala la beki wao Mohammed Fakhi.

Habari zinasema kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa wakisema kwamba hawakushirikishwa kuandika barua TFF kupinga uamuzi wa Kamati ya saa 72 ambayo iliipoka Kagera pointi tatu kwa kumchezesha beki huyo akiwa na kadi tatu za njano kwenye mechi ya Simba.

“Barua hii imeandikwa kwa shinikizo kutoka nje ya Kagera Sugar. Watu wamepiga simu na kusema andikeni barua ya malalamiko itafanyiwa kazi,” kimesema chanzo chetu kikimkariri mmoja wa viongozi wa Kagera Sugar.

Kama vile haitoshi, siku chache baada ya Kamati ya saa 72 kupitia mwenyekiti wake, Hamadi Yahaya kutangaza kuwa Simba imeshinda malalamiko yake, kocha wa Kagera Sugar Mecky Mexime alitupa lawama kwa viongozi wa soka Mkoa wa Kagera.

Mexime amesema viongozi wa mkoa huo wamekuwa wanafiki kwa kuzisaidia timu ambazo wanazipenda kwa kutoa kile alichokiita kuwa ni “siri” za Kagera Sugar.

Amesema, suala la kadi tatu za njano za Mohammed Fakhi ni wazi limeibuliwa na kiongozi mmoja wa mkoa huo ambaye amekuwa akiiombea mabaya kagera Sugar.


Mmoja wa watu wa karibu na timu hiyo amesema kwamba kumekuwa na utata mkubwa wa kukubaliana kuhusu malalamiko hayo na kwamba kuna mambo yalifunikwa kabla ya kuibuliwa upya.           

No comments