KOCHA LWANDAMINA ASUKA MIPANGO MAALUM ILI KUIVUSHA YANGA SC KWENYE MAFANIKIO

PAMOJA na kipindi kigumu ambacho klabu ya Yanga inapitia hivi sasa, kocha wa timu hiyo George Lwandamina raia wa Zambia amesema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha timu hiyo inavuka mafanikio waliyoyapata kutoka michuano ya CAF msimu uliopita.

Yanga ilitolewa na Zanaco katika michuano ya klabu bingwa Afrika baada ya kutoka sare ya 0-0 kwenye uwanja wa National Heroes Lusaka huku mchezo wa awali ikimalizika kwa mabao 1-1 March 11.

“Nina mpango wa kubadilisha hali ya mambo kwa haraka klabuni na kurejesha hali ya umoja na ushindi ili kufikia mafanikio yaliyopatikana msimu uliopita,” alisema Lwandamina.

“Nyota wengi wa kikosi cha kwanza wametoka kwenye majukumu ya kuzitumikia timu za taifa lakini hilo haliwezi kuadhili programu yangu.”

“Siangalii ukubwa wa timu niliyopangiwa badala yake natazama kile ambacho naweza kukifanya kwa ajili ya kuipa Yanga mafanikio,” aliongeza.

“Hatuna kikosi kibaya, tunashiriki michuano ya Kombe la CAF tukiamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi, robo fainali na hata zaidi ya hapo,” aliongeza.

Lwandamina alifanikiwa kuifikisha klabu ya Zesco United katika hatua ya nusu fainali msimu uliopita na kufanya timu hiyo kuwa ya kwanza kufika hatua hiyo katika michuano ya Kombe la CAF kwa klabu za Zambia.

No comments