KOCHA WA ZAMANI WA SIMBA ASIFU KIKOSI CHA MWAKA HUU... ashauri kisibomolewe msimu ujao


SIMBA ina kikosi bora katika msimu huu wa Ligi na Wekundu hao wameshauriwa kutokipangua kikosi hicho katika usajili wa msimu ujao.

Katika kujionyesha inajipigia debe, kocha aliyeifundisha Simba miaka ya nyuma na ambaye msimu huu alikuwa kocha wa Stand United ya Shnyanga, Patrick Liewing, amesema Simba ina kikosi imara kabisa.

Liewing amesema katika mahojiano na saluti5 kwamba kama angekuwa kocha wa Simba angeshauri kikosi hicho kisibomolewe.

Liewing amesema badala ya kumoboa kikosi hicho kama watu wengine wanavyotaka, Simba ingefanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo na hasa kwenye safu ya ushambuliaji.

Mfaransa huyo amesema hata hivyo Simba inahitaji kuwa na straika mwenye nguvu na msumbufu badala ya kuwategemea washambuliaji wake wa sasa ambapo wanatumia akili zaidi.

“Ukiwatazama washambuliaji wa Simba ni wazuri lakini pale inapohitajika nguvu ya ziada wanashindwa kufanya maamuzi. Pale ndipo panatakiwa kufanyiwa mabadiliko,” amesema.

Liewing amesema kwamba mshambuliaji Frederick Blagnon ana nguvu nyingi lakini amekuwa akishindwa kufanya maamuzi wakati ambapo Simba inahitaji mabao.

“Kama ningekuwa kocha wa Simba ningetafuta washambuliaji wawili tu wa kumsaidia Ibraimu Ajibu na Laudit Mavugo ambao wanatumia akili nyingi zaidi,” amesema Liewing ambaye ndiye aliyewaibua Ajibu na Jonas Mkude.

“Mimi siyo kocha wa Simba lakini nadhani kuna mambo madogo tu yanayotakiwa kuboreshwa ili Simba ibaki katika uimara wake,” amesema.

Liewing ndie aliyetengeneza mfumo wa kuwaamini vijana katika kikosi cha Simba badala ya kuwategemea wachezaji ambao umri unakimbia.

No comments