MAANDALIZI YA UMISETA YAANZA KWA SEMINA DODOMA

MAAFISA Elimu wa mikoa wamenufaika na semina elekezi ya maandalizi ya michezo ya shule za sekondari (UMISETA), iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa chuo cha mipango mjini Dodoma.

Semina hiyo iliandaliwa na serikali kupitia Baraza la Taifa la Michezo (BMT), kwa kushirikiana na kampuni ya vinywaji baridi Cocacola kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Hayo yameelezwa na Ofisa Habari wa BMT, Najaha Bakari.
Alisema kuwa, semina hiyo itasaidia kutimiza hatua ya serikali kuendeleza michezo kuanzia ngazi mbalimbali, hivyo ni kozi iliyo na malengo makubwa kwa wakati wa sasa na baadae.

Alisema kuwa semina hiyo ni viashiria vya kuanza kwa maandalizi ya michezo kwa shule za sekondari yaani UMISETA, ambayo yalisimamishwa.

“Semina hii ni moja ya viashiria vya kutoa maelekezo kwa watendaji ambao ni maafisa michezo pamoja na elimu, ili waweze kuanza maandalizi kwa mashindano ya mwaka huu,” alisema.


Mashindano hayo ya UMISETA yamekuwa yakisaidia kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wadogo wanaoanza kushiriki katika ngazi za shule, wilaya, mkoa hadi taifa. 

No comments