METHOD MWANJALI AANZA MAZOEZI NA WENZAKE SIMBA SC... benchi la ufundi lasema hana nafasi katika mechi zilizosalia

BEKI wa Simba raia wa Zimbabwe, Method Mwanjali ameanza mazoezi na wenzake katika kambi ya wekundu hao mjini Morogoro.

Hata hivyo, benchi la ufundi la Simba limeweka wazi kuwa beki huyo hana nafasi kwa sasa katika mechi hizi zilizobaki.

Mzimbabwe huyo amekaa nje ya dimba kwa takriban miezi miwili sasa akiuguza majeraha ya goti na benchi la ufundi la timu hiyo limeamua kumuondoa rasmi kwenye mipango yao katika mechi zao za kumaliza msimu huu.

Mwanjali ambaye aliumia Februari 11, mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Prisons ambao Simba waliibuka na ushindi wa mabao 3-0, tangu siku hiyo hakuweza kuitumikia tena timu hiyo mpaka leo akiwa anaendelea kupata matibabu ya majeraha yake.

Jackson Mayanja ambaye ni kocha msaidizi wa kikosi hicho, amesema; “Huyo kwa sasa usimuhesabie kwanza kwani bado anapatiwa matibabu na hivi hata kama akipona sasa hivi hawezi kucheza kwasababu hatakuwa fiti.”

“Kwa kitendo chake cha kukaa nje miezi miwili bila ya kucheza, kitaalamu na kiufundi itakuwa ni vigumu kucheza kwa sasa kwani ukiangalia mechi zilizosalia si za kujaribu wachezaji, hivyo Mwanjali kwa sasa atapumzika.”

Hata hivyo beki huyo ameanza mazoezi ingawa amekuwa chini ya usimamizi wa daktari wa Simba, Yassin Gembe.

Katika mazoezi ya Simba yanayoendelea mkoani Morogoro, ni wachezaji wawili pekee ambao wamekosekana kwenye kikosi hicho kutokana na kuwa majeruhi.


Wachezaji hao ni beki wa kulia, Hamadi Juma pamoja na kiungo mshambuliaji, Jamal Mnyate na wameachwa jijini Dar es Salaam.

No comments