MSONDO NGOMA ‘YAREJESHWA’ ENZI ZA NUTA, JUWATA, OTTU JAZZ ...TUCTA Jazz Band yanukia


Msondo Ngoma Music Band huenda ikabadili jina na kuitwa TUCTA Jazz Band iwapo mazungumzo yanayoendelea yatafikia muafaka.

Inadaiwa kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Trade Union Congress of Tanzania -TUCTA) zamani ikijulikana kama NUTA, JUWATA, OTTU, TFTU inataka kuirejesha mikononi mwao bendi hiyo.

Msondo ilimilikiwa na NUTA, JUWATA, OTTU na wakati shirikisho hilo likibadili muundo na kuwa TFTU zaidi ya miaka 20 iliyopita, likaibinafsisha bendi na ikabakia chini ya umiliki wa wanamuziki waandamizi baadhi yao wakiwemo Said Mabela, Roman Mng’ande pamoja na TX Moshi William, Athuman Momba Joseph Maina na Maalim Gurumo ambao wametangulia mbele ya haki.

Kupitia kumilikiwa na shirikisho la wafanyakazi, Msondo iliyoanzishwa mwaka 1964, ikapitia majina ya NUTA Jazz Band, Juwata Jazz Band, OTTU Jazz Band kabla ya kuitwa Msondo Ngoma Music Band linalotumika hadi hivi sasa.

Mmoja wa waimbaji wa Msondo Ngoma Hassan Moshi (TX Junior), ameandika kwenye ukurasa wake wa facebook: “Safarini tukielekea moshi tucta jazz band msondo ngoma yawatanzania band rasmi imerudi serikarini kwenye chama cha wafanyakazi tucta tukutane mayday moshiii”.


Hassan Moshi akasindikiza maandishi yake na picha ya bus dogo lililondikwa ubavuni TUCTA Jazz Band.

Hata hivyo meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti ameiambia Saluti5 kwa njia ya simu kuwa bado hawajafikia muafaka.

“Ni mapema mno kusema lolote kwa sasa. Kuna mazungumzo yanaendelea lakini bado hatujafikia muafaka,” alisema Kibiriti.

No comments