MTIBWA SUGAR YAKANUSHA UVUMI WA KUSHINDWA KULIPA MISHAHARA YA WACHEZAJI WAO

KUFUATIA uvumi ulioenea kwa wadau wa soka kuwa klabu ya Mtibwa imeshindwa kuwalipa mishahara wachezaji, uongozi wa timu hiyo ya Manungu Turiani Morogoro umeibuka na kukanusha madai hayo.

Ofisa habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru alisema kuwa, yote yanayozungumzwa hayana ukweli wowote kwani tayari walishamalizana na wachezaji wote.

“Sijui kwanini watu hupenda kutunga maneno yasiyokuwa na ukweli wowote, labda nikuhakikishie kwamba hakuna mchezaji yeyote ambaye anaidai Mtibwa, kila mtu alishalipwa stahiki yake,” alisema Ofisa huyo.

“Mtibwa ni klabu kubwa, hakuna na wala hatujawahi kuwa na tatizo la mshahara kwa wachezaji wetu, hivi sasa timu ipo kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi zilizosalia za Ligi,” aliongeza.

Mtibwa inakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuzipisha mbio za ubingwa kwa timu za Simba na Yanga ambazo zinafukuzana kileleni. 

No comments