MWAMUZI MTANZANIA APEWA SHAVU AFCON U17

MWAMUZI wa Tanzania, Frank John Komba amekuwa miongoni mwa waamuzi waliopata nafasi ya kuchezesha kwenye michuano ya Afrika kwa vijana mwenye umri chini ya miaka 17 inayotarajia kufanyika nchini Gabon.

Komba atasimama kama mshika bendera kwenye michuano hiyo itakayofanyika nchini Gabon ambako timu ya taifa ya vijana, Serengeti Boys itakuwa ikishiriki pia.

Mwamuzi huyo msaidizi ataungana na waamuzi wengine kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati wakiwemo Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi na Davies Ogenche Omweno mwamuzi wa kati kutoka nchini Kenya.

Umekuwa ni mwaka wa neema kwa Tanzania baada ya kuwa na wawakilishi Serengeti Boys kwenye michuano hiyo ambapo kwa sasa imepiga kambi ya mwezi mmoja nchini Morocco na baada ya hapo itaenda nchini Cameroon kwa kambi ya wiki moja.


Vijana hao wameonekana kuendelea vyema na mazoezi yao chini ya kocha mzawa Bakari Shime ambapo rais wa TFF Jamal Malinzi aliyekuwa nchini Morocco hivi karibuni amewapa hamasa kwamba ikiwa watafanikiwa kuwa mabingwa wa michuano hiyo, fedha zote watakazolipwa watagawana wachezaji na benchi la ufundi.

No comments