MWANASOKA WA KENYA ALIYETISHIWA MAISHA AFRIKA KUSINI AFUNGUKA ZAIDI

MWANASOKA wa kimataifa wa Kenya, Clifton Miheso ambaye amedai kutishiwa maisha nchini Afrika Kusini, ameomba msaada wa FIFA kuamua haraka shauri lake.

Juzi mwanasoka huyo alikuwa amewasilisha rasmi malalamiko katika shirikisho la soka duniani (FIFA), akidai kwamba alilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kuhitimisha mkataba wake katika klabu ya Golden Arrows.

Miheso anadai kwamba kisa hicho kilitokea Januari 14, katika ofisi za klabu hiyo mjini Durban nchini Afrika Kusini.
Mchezaji huyo mwenye miaka 24 anataka Golden Arrows ipigwe marufuku kununua au kuuza wachezaji au wapewe adhabu nyingine yoyote ile.

Aidha, anataka alipwe jumla ya dola 22,000 ambazo anasema anaidai klabu hiyo kama ujira wake.

Golden Arrows imekanusha tuhuma za mchezaji huyo lakini wakakataa kuzungumzia zaidi kisa hicho.

Mwakilishi wa winga huyo anasema klabu hiyo haikutoa maelezo yoyote ya kuridhisha kuhusu kisa hicho.

Miheso ameyeichezea timu ya taifa ya Kenya na kufunga mabao matano.

No comments