"SERENGETI BOYS INA UWEZEKANO MKUBWA WA KUIBUKA NA UBINGWA WA KOMBE LA AFCON MWAKA HUU"

MCHEZAJI wa zamani wa timu ya Tanzania Prisons, Osward Morris ambaye hivi sasa ni Katibu wa Serengeti, amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kikosi hicho kuibuka na ubingwa wa Kombe la AFCON mwaka huu kutokana na maandalizi yanayoendelea kufanyika.

Morris alisema kuwa hata kundi B walilopangwa, lenye timu za Angola, Ethiopia na Nigeria halitishi sana, lakini pia michuano yenyewe inashirikisha timu chache tofauti na ile ya wakubwa.

“Ubingwa naona wala ni suala ambalo linawezekana kabisa kwasababu kundi tulilopangwa halitishi sana na hata idadi ya mechi tutakazocheza sio nyingi kama ilivyo kwenye michuano ya wakubwa,” alisema Morris.

“Hata maandalizi tunayofanya na kambi tuliyoko ni ya hali ya juu, hivyo naona kuna kila dalili ya kuibuka na ubingwa, Watanzania wanatuunga mkono lakini hata Shirikisho limetoa hamasa kubwa kwa vijana,” aliongeza veteran huyo.

Michuano ya AFCON kwa vijana inatarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28, katika miji ya Librevile na Port Gentil nchini Gabon huku bingwa akiondoka na kitita cha dola za Kimarekani 75,000 ambazo ni sawa na sh. mil 165 za Tanzania.


Hata hivyo, katika kuitia hamasa timu hiyo, rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema fedha hiyo yote watagawana wachezaji na benchi la ufundi ikiwa watafanikiwa kuibuka na ubingwa huo.

No comments