SIMBA SC YAIKATA MAINI YANGA... Mkude, Ajib sasa kubaki Msimbazi hadi 2019

SIMBA imemalizana na wechezaji wake wawili muhimu waliokuwa wakidaiwa kutakiwa na Yanga, nahodha Jonas Mkunde na Ibrahim Ajib, imefahamika.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kwamba wachezaji hao wawili wameongezewa mikataba ya miaka miwili kila mmoja na hivyo kuwa na uhakika wa kubaki Simba hadi mwaka 2019.

Habari hizo zinasema kwamba habari ya kuondoka kwa wachezaji hao ni kama imekufa rasmi baada ya kupewa mikataba mipya.

“Kama kuna watu walikuwa wanavizia kuwaona wachezaji hao wamemaliza mikataba na kuhamia Yanga, basi wajue kwamba Yanga ya sasa haina ubavu wa kumsajili mchezaji wa Simba, labda mchezaji huyo ahamie kwa mapenzi yake mwenyewe,” kimesema chanzo hicho.

Lakini pia habari zinasema kwamba licha ya wawili hao kupewa mikataba ya miaka miwili kila mmoja, pia mikataba kwa wachezaji wengine ambao wanamalizia muda wao tayari iko mezani.

“Sio hao wawili tu, kuna wachezaji wengine mikataba yao inakaribia kumalizika nao wameshaandaliwa mikataba yao, na mambo mengi yameboreshwa,” amesema mtoa habari wetu.

Ajib na Mkude wamekuwa wakihusishwa na kuhamia Yanga na kwamba kigogo mmoja serikalini amekuwa akituhumiwa kuwarubuni wachezaji hao.

Lakini pia kulikuwa na taarifa kwamba wachezaji hao wanajihandaa kuhamia katika timu iliyopanda Ligi Kuu ya Singida United ya mkoa wa Singida.

Mikataba hiyo mipya hata hivyo imeweka nafasi kwa wanasoka hao kama watapata timu ya kucheza nje ya Tanzania kwenda kujaribu maisha huko.


“Hapa maana yake ni kwamba Simba itakuwa na uhakika wa kuuza wachezaji wake nje kama ilivyo utamaduni wake na hivyo kuendelea kuingiza pesa kutokana na wachezaji,” chanzo hicho kimesema.

No comments