SIMBA YAPOTEZEA POINTI TATU WALIZOPOKWA KWA "MDOMO"... yang'ang'ania barua rasmi kutoka Kamati ya Sheria

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema hauwezi kuzungumzia kitendo cha wao kupokonywa pointi tatu na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji mpaka hapo watakapopewa nakala ya maamuzi ya kikao cha Kamati hiyo.

Makamu wa rais wa Simba, Godfrey Nyange “Kaburu” alisema wamesikia taarifa kupitia mitandao na vyombo vingine mbalimbali vya habari kuwa wamepokwa pointi walizopewa na Kamati hiyo.

“Habari hizo zilizotolewa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambazo zinaonyesha kutozingatia kanuni na taratibu katika kupokonya pointi zetu, kiukweli zina upungufu mkubwa,” alisema Kaburu.

Aidha, Kaburu alisema wanashangazwa na kitendo cha Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa kukiri kuwa mchezaji wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi alikuwa na kadi tatu za njano hivyo kuamua kuinyang’anya pointi kutokana na kutotimiza baadhi ya vigezo wakati wa kudai haki yao.

Alisema, anashangaa kuona TFF inashindwa kutimiza majukumu yao wenyewe pasipo kusubiri klabu ziende kupeleka malalamiko na ndipo waweze kuchukua maamuzi wanayopaswa kuyachukua.


“Hili suala lipo wazi kutokana na wao wenyewe kukiri kwamba Fakhi alikuwa anakuwa ana kadi tatu za njano pasipo kujali kama sisi tumekata rufaa au la, pia hatujajua ni mambo gani yanayoendelea kwa sababu hadi hivi sasa hatujapata barua rasmi inayotueleza kile kilichofanyika kwa siku zote ambapo Kamati ya Sheria, katiba na Hadi za Wachezaji walijadili kwa siku zote,” alisema Kaburu.

No comments