SIMBA YASHANGAZWA NA MADAI YA KUMNUNUA KIPA WA MBAO FC KWENYE MECHI DHIDI YAO

KLABU ya Simba imesema kwamba timu ya Mbao FC ya Mwanza imemwonea bure kipa wao, Erick Ngwengwe kumsimamisha kwa madai ya kuhongwa na Simba katika mechi yao ya hivi karibuni.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe amesema kwamba Simba imeamua kuwekeza pesa kwa wachezaji wake na haiwezi kushiriki michezo michafu ya kununua mechi.

Mwenyekiti huyo amesema kwamba Simba inashangazwa na taarifa kuwa Mbao FC imemsimamisha kipa wao huyo msomi kwa madai kwamba ushindi ambao Simba umeupata wa mabao 3-2 dhidi ya timu hiyo ya Mwanza umetokana na kipa huyo kununuliwa.

Amesema kwamba, wapinzani wao wanaowatuhumu kwamba wanatoa rushwa, wanakosea kutokana na wao kutumia fedha kwa wachezaji wao kwa ajili ya kuongeza morali ya kusaka ushindi.

Hivi karibuni Simba walituhumiwa kutoa rushwa kwa ajili ya kuwarubuni wachezaji wa Mbao FC baada ya kutoka nyuma ya mabao 2-0 na kushinda 3-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa uwanja wa Kirumba, Mwanza.


Kutokana na tuhuma hizo, viongozi wa Mbao kupitia Mwenyekiti wake, SollyNjoshi walimsimamisha kipa wao, Eric Ngwengwe ambaye alidaka kwenye pambano hilo.

No comments